Vodacom na Nokia zaingia katika ushirikiano kupunguza gharama za simu.

*Ushirikiano huo ni katika kuwanufaisha vijana.
*Ofa ya simu ni Nokia Asha 200 na Niokia Asha 302
*Wateja kupata ya intanet bure kwa miezi sita, huduma ya facebook, twitter na Wikipedia kuendelea kuwa bure.

Dar es Salaam, Julai 18, 2012 ... Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imeingia katika ubia na kampuni ya Nokia katika kutoa ofa ya aina mpya ya simu za Nokia kwa Watanzania.

Aina ya simu ambazo zimeingizwa katika ofa hiyo mpya ni simu aina ya Nokia Asha 200 na Nokia Asha 203 ambazo ni katika mpango maalum wa Vodacom wa kupunguza gharama za huduma za simu kwa vijana.

Kupitia simu hizo, wateja wataweza kupata huduma nafuu kwa simu ya Nokia Asha 200 inayouzwa kwa shilingi 149,999 na watapata muda wa bure wa maongezi na MB 125. Kwa simu ya Nokia Asha 302 inayouzwa kwa shilingi 219,000 wateja watapata MB 500 kwa miezi sita mfululizo baada ya kuweka muda wa maongezi wa Shilingi 1000, 2000, au 5000 huku huduma ya facebook, twitter na Wikipedia zikiendelea kuwa bure.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa ofa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Vifaa wa kampuni ya Vodacom Tanzania Bw. Mngopelinye Kiwanga, amesema kuwa ofa hiyo inalenga kuongeza soko kwa kampuni hiyo na kukuza utoaji wa huduma na uuzaji wa bidhaa, na kuongeza kuwa vijana, ambao wanachukua idadi kubwa ya watu katika taifa, ni vyema wakapata huduma nafuu za mawasiliano ili kuchangia katika ukuaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"Tunaamini kwa mpango huu, tutawafikia wateja wengi zaidi iwezekanavyo," alisema Kiwanga, na kuongezea kuwa kutakuwa na maboresho mbalimbali ya mtandao na ubora wa bidhaa, suala litakalo wawezesha wateja kufikiwa na huduma na kutanabaisha kuwa zipo ofa nyingi na bidhaa ambazo kampuni hiyo inatarajia kutoa kwa wateja wake ndani ya Mwaka huu.

" Napenda kuwahakikishia wateja wetu kuwa tutaendelea kuboresha na kuleta huduma nzuri na bora kwa ajili yao ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku na kuwa na mahusiano mazuri na wateja wetu," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Nokia Tanzania Samson Majwala, amesema kuwa simu hizo zina sifa nzuri na ni rahisi kuzitumia, suala ambalo litawavutia watu wengi kununua na kuzitumia kwa urahisi.

"Simu hizi ni nzuri na rahisi kutumia. Nina imani kuwa wateja watafurahia na kuzitumia," alisema Majwala.